Wekundu wa Msimbazi Simba wapo kwenye mazungumzo na viungo wakabaji watatu kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutibu tatizo la nafasi hiyo ambalo limekua ni la muda mrefu.
Simba SC ambayo licha ya kwamba hajathibitisha rasmi, lakini taarifa zimedai imeshawasainisha wachezaji wawili raia wa Cameroon, winga wa kushoto, Lendre Onana aliyekuwa akiichezea Rayon Sport ya Rwanda na beki wa kati, Che Fondoh Malone kutoka Cotton Sport, huku pia ikidaiwa kuwa kwenye hatua za mwisho kumsajili Mlinda Lango Mbrazil, Caique Luiz Santos anayekipiga na Ypiranga SC, lakini kwa sasa ikigeukia eneo la kiungo mkabaji.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimesema kuwa iko kwenye mazungumzo na wachezaji watatu wanaocheza eneo hilo, ambao ni Efoe Novon kutoka ASKO Cara ya Togo, Harvy Ossete raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayeichezea FC Saint Eloi Lupopo, na Banfa Sylla wa MAS Fes ya Morocco.
Hata hivyo, inadaiwa mabosi wa Simba SC na Kocha wao, Robert Oliveira, wanavutiwa zaidi na Sylla, ambaye thamani yake inatajwa kuwa ni dola za Kimarekani 170,000 ili kuvunja mkataba kwa klabu yake.
“Lengo ni kumpata Sylla, lakini hawa wengine nao si wabaya, ni wachezaji wazuri sana na tumewajumuisha ikiwa ni kama mbadala iwapo dili halitofanikiwa, kwenye soka kuna mambo mengi, mnaweza kuongea vizuri, lakini mwishoni mambo yasiende vizuri, uzuri ni kwamba wote wameshazungumza nao,” kimesema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Chanzo hicho kimesema kutokana na muda kuwa mfupi, imebidi wafanye haraka kumaliza usajili ili kikosi kiingine kambini mara moja kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya (Pre Season), hivyo wamewaweka tayari wachezaji wote hao watatu ili sehemu moja ikishindikana, basi mwingine anachukua nafasi.
“Hatutaki kurudia makosa ya msimu uliopita unamkosa huyu, unaanza tena mazungumzo na mtu mwingine, yanakuwa marefu mpaka kikosi kinaanza maandalizi ya msimu ujao bado hatujamaliza kusajili, tunataka mwalimu akianza awe na wachezaji wote anaowahitaji,” chanzo kimebainisha.
Simba SC inataka kutibu tatizo sugu la kiungo mkabaji ambapo kwa sasa inawategemea wachezaji wawili tu, Sadio Kanoute raia wa Mali na Mtanzania Mzamiru Yassin ambao hata hivyo, wataalamu wa soka wanasema si viungo wakabaji asilia, badala yake ni wasaidizi wa viungo wakabaji wanaocheza juu kidogo.
Tangu kuondoka kwa Mbrazil James Kotei, Gerson Fraga na Thadeo Lwanga, ambao ndiyo viungo wakabaji asilia, Simba SC imekuwa na tatizo hilo ambalo limekuwa likiigharimu katika baadhi ya mechi.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema safari hii hawataki tena kufanya makosa yaliyowagharimu ndiyo maana wanasajili wachezaji ambao wana mikataba na klabu zao.
Amesema pesa kwao si tatizo na kwamba watamnunua mchezaji yeyote kwa gharama yoyote kutoka mahala popote.
“Mzigo upo, tutamsajili yeyote yule, mradi tu kocha Robertinho (Robert Oliveira) amempendekeza,” amesema.
Kwa mujibu wa Ahmed Ally, kuanzia leo Jumatatu (Julai 03) klabu hiyo inaweza kuanza kutangaza wachezaji ambao imeshawasajili mpaka sasa.