Uongozi wa Simba SC umeichimba Mkwara klabu ya CD Primeiro de Agosto (Clube Desportivo 1º de Agosto), kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa hatua ya Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Miamba hiyo itapapatuana kati ya Oktoba 07-09 mjini Luanda nchini Angola, baada ya kufuzu hatua ya awali, ambapo CD Primeiro de Agosto iliiondoa Red Arrows ya Zambia kwa ushindi wa jumla 2-1, huku Simba SC ikiifurumisha Nyasa Big Bullet ya Malawi kwa ushindi wa jumla wa 4-0.
Simba SC imetuma salamu hizo nchini Angola kwa kuwataka CD Primeiro de Agosto kuwa wataarabu na katu wasijaribu kufanya vitendo vya kihuni kuanzia ndani hadi nje ya uwanja, kwani hawatakaa kimya, ni lazima watajibu mapigo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema uongozi unafahamu uhuni wote wanaoufanya CD Primeiro de Agosto, wanapokua kwao Angola, hivyo wamejiandaa kupambana nao.
Amhed amesema kamwe hawatavumilia vitendo vya kihuni watakavyovifanya wapinzani wao wakiwa nchini Angola, badala yake watalipiza huko ugenini kabla ya kurudiana hapa nyumbani.
Ameongeza kuwa, uongozi umejipanga katika kila kitu kitakachotokea ugenini baada ya kuanza maandalizi ya kuhakikisha wanapambana na kila hujuma itakayotokea.
“Tumepanga kuwahi mapema Angola kwa maana ya viongozi kuandaa mazingira mazuri itakayofikia timu kwa maana ya hoteli, uwanja wa kufanyia mazoezi pamoja na chakula.
“Hiyo ni baada ya kuujua uhuni wote kwa maana ya hujuma wanazotumia, kama uongozi tumejiandaa na kila uhuni watakaoufanya wa ndani na nje ya uwanja.
“Hivyo wakae wakijua kwamba hatutavumilia kwa kila uhuni watakaoufanya mara baada ya kuingia katika ardhi ya Angola, tena wasijaribu kabisa kingine wafahamu kabisa lazima na wao waje hapa nchini,” amesema Ally.
Simba SC itakutana na CD Primeiro de Agosto kwa mara ya kwanza katika historia yake ya kushiriki Michuano ya Kimataifa Barani Afrika, lakini imewahi kukutana na klabu ya Angola CRD Libolo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu wa 2012/13.
Katika mchezo huo Simba SC ilikubali kufungwa 1-0 nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa (17/02/2013), kisha ikapoteza kwa kufungwa 4-0 ugenini (03/03/2013).