Kikosi cha Simba SC kimeondoka Jijini Dar es salaam leo Jumanne (April 05) majira ya mchana kuelekea Jijini Tanga, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 18 wa ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.
Simba SC ambayo ndio Bingwa Mtetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, itakua mgeni wa Coastal Union keshokutwa Alhamis (April 07) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema kikosi chao kimeondoka salama na wana matarajio ya kufanya vizuri katika mchezo huo utakaoanza saa kumi jioni.
Amesema Kikosi chao kimeondoka na Morari ya hali ya juu, baada ya kumalizana na USGN katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kutinga hatua ya Robo Fainali kwa ushindi wa mabo 4-0 juzi Jumapili (April 03).
“Kikosi kimeondoka jijini Dar es salaam leso mchana kuelekea Tanga, tunaamini mchezo utakua mzuri na matumaini kwa upande wetu ni ushindi ambao utaendelea kutusogeza katika lengo la kutetea ubingwa wetu.”
“Wachezaji wameondoka wakiwa na Morari ya hali ya juu, baada ya kumalizana na USGN juzi Jumapili na kutinga Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, tunaihamishia Pumzi ya Moto katika Ligi Kuu na kwa bahati mbaya Coastal Union wanakua wakwanza kukutana nayo.” amesema Ahmed Ally
Katika hatua nyingine Ahmed amesema baada ya mchezo huo, Simba SC itaelekea Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania na baadae watakwenda mkoani Geita kupapatuana na Geita Gold FC.