Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kimeondoka Jijini Dar es salaam, kuelekea mkoani Kagera tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kegera Sugar kesho Jumatano (Januari 26).

Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 25, imeondoka kwa usafiri wa ndege, huku ikiwa na matumaini ya kwenda kupambania alama tatu za mchezo huo wa kiporo.

Mchezo huo ulipaswa kuchezwa Desemba 12 mwaka 2021, lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi kutokana na wachezaji wengi wa Simba SC kukutwa na maambukizo ya ugonjwa wa mafua, kukohoa, kichwa na homa kali, hivyo kusababishwa mechi isifanyike kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Mwishoni mwa juma lililopita Jumamosi (Januari 22) Simba SC ilicheza dhidi ya Mtibwa Sugar na kuambulia matokeo ya sare 0-0, na kabla ya mchezo huo ilikua mjini Mbeya na iliambulia kisago cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

Kagera Sugar wao waliibanjua Dodoma Jiji FC nyumbani kwao Dodoma mwishoni mwa juma lililopita Jumamosi (Januari 22), kwa ushindi wa 2-1.

Mazingira ya matokeo ya timu hizo, yanachochea chachu ya ushindani mkubwa ambao utaleta mpambano mkali ndani ya dakika 90 kwenye Dimba la Kaitaba kesho Jumatano (Januari 26).

Kocha Simba SC atamba kurejesha furaha Msimbazi
Kagera Sugar waitambia Simba SC