Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC mapema hii leo waliwasili jijini Mbeya, ikiwa ni sehemu ya safari ya kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Al-Khamis Oktoba 22, Uwanja wa Nelson Mandela uliopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Simba itaweka kambi kwa siku mbili jijini Mbeya, na baadae itaendelea na safari ya kuelekea mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.

Msafara wa mabingwa wao watetezi umejumuisha wachezaji 22 huku nahodha na mshambuliaji Jonh Bocco ambae anaendelea na mazoezi mepesi baada ya kupona majeraha, kiungo kutoka Brazil Gerison na mshambuliaji Meddie Kagere (majeruhi), wakiachwa Dar es salaam.

Kwa mantiki hiyo mshambuliaji kutoka DC Congo Criss Mushimba Koppe Mugalu, atakua na jukumu la kupambana na safu ya ulinzi ya maafande Tanzania Prisons kwenye mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa.

Hata hivyo mshambuliaji huyo tayari ameshaonyesha umahiri wake kwa kupachika mabao kila anapopewa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Simba hivyo, na kujiwekea imani kubwa kwa benchi la ufundi na mashabiki.

Kocha mkuu  Sven Vanderbroeck amesema: “Tumeondoka na wachezaji 22 ambao tunaamini wanatosha kwa ajili ya mchezo huo ambapo wote wako vizuri kiafya tayari kuipigania timu.

“Pia Mchezo dhidi ya Prisons tunaamini utakuwa mgumu kama zilivyo mechi nyingine za ugenini. Wao wanacheza soka la lenye matumizi makubwa ya nguvu lakini tumejiandaa kuwakabili.

“Hatujaondoka na kikosi kizima badala yake tumesafiri na wachezaji 22 kwa ajili mechi hii, matumaini ya kufanya vizuri ni makubwa na tutahakikisha tunafanikiwa.”

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 13 sawa na Young Africans, lakini utofauti wa mabao ya kufnga na kufungwa unawaweka wananchi kwenye nafasi ya tatu.

Mzawa aweka rekodi Ligi Kuu 2020/21
Kaze: Ninawaamini Sogne, Sarpong