Uongozi wa Klabu ya Simba SC umewahimiza Mashabiki na Wanachama wake kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuishangilia timu yao pasina kuchagua michezo, ili kuiwezesha Klabu hiyo kuwa na mapato makubwa ya milangoni kupitia Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wamekua na muitikio mdogo kufika Uwanjani hapo pindi timu yao inapokuwa na mtihani wa kucheza nyumbani kwenye Michezo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, tofauti na wanavojitokeza kwenye Michuano ya Kimataifa.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, ameweka hadharani ombi la kuwataka Mashabiki na Wanachama wao kubadili mfumo, na kuanza kwenda Uwanjani hasa wanapocheza Nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ahmed Ally ameweka ombi hilo akiwahimiza Mashabiki na Wanachama kuanza kuonyesha tofauti ya kufika Uwanja wa Mkapa kuanzia mchezo wa Jumapili ambapo kikosi chao kitapapatuana na Dodoma jiji FC mishale ya saa moja usiku.
Ahmed ametumia Kurasa zake za Mitandao ya Kijamii kuandika ujumbe wenye ombi hilo: Moja ya tatizo ambalo tunapaswa kulitatua ni mashabiki wa Simba kutoenda uwanjani kwenye mechi zetu za nyumbani.
Idadi ya wanaoingia uwanjani kwenye mechi za nyumbani ni ndogo mnoo.
Wengi tunaenda uwanjani kutokana na ukubwa wa mechi au ukubwa wa mashindano ndo maana ni rahisi kujaza uwanja kwenye derby au mechi za kimataifa.
Ukienda Old Trafford mechi ya Manchester na Arsenal inajaza uwanja na mechi Manchester na Watford inajaza uwanja hapa mashabiki hawafuati mpinzani wanaifuata timu yao na hiki ndo kilio changu.
Mfano mechi yetu dhidi ya Geita Gold tulipata mapato ya Shilingi Milioni 14 tu.
Ni pesa ndogo mnoo kwenye mpira wa miguu.
Kama tunaingiza Milioni 14, kwa mechi 14 za nyumbani tutavuna milioni 210 pesa ambayo haitoshi hata mishahara ya mwezi mmoja.
Ni rahisi kumsikia mtu anasema kama hamna pesa ya usajili semeni tuchange.
Kuchangishana sio njia ya kudumu ya kuendesha klabu, njia ya sahihi klabu kupata fedha ni mapato ya mlangoni na yanapatikana kwa sisi mashabiki kuja kwa wingi mechi za nyumbani.
Tukutane kwa Mkapa Jumapili tuanze kuvunja huu mwiko ?
SEMAJI LA CAF