Aliyekuwa Kocha Msaidizi Al Ahly ya nchini Misri, Cavin Johnson amesema Orlando Pirates itakabiliwa na wakati mgumu mno itakapocheza na Simba SC kwenye hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika, huku kwa mara ya kwanza Tanzania itatumia VAR kwenye Uwanja.

Simba SC imepangwa kucheza na Orlando Pirates kwenye hatua hiyo baada ya kuitoa US Gendamarie ya Niger kwa ushindi wa 4-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, Jumapili (April 03).

Kwenye mchezo huu mwamuzi wa kati atakuwa ni Haythem Guirat kutoka Tunisia, akisaidiwa na mwamuziki msaidizi namba moja, Khalil Hassani (Tunisia), mwamuzi namba mbili Samuel Pwadutakam (Nigeria) na mwamuzi wa akiba ni Sadok Selmi (Tunisia).

Mwamuzi wa teknolojia ya usaidizi kwa njia ya video (VAR) atakuwa ni Ahmed Alghandour (Misri) na msaidizi wake ni Youssef Elbosaty (Misri) na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuitumia.

Katika mkutano wake na waaandishi wa habari wa Afrika Kusini, Johnson amesema itakuwa vigumu sana kwa Pirates na sio kitu rahisi kwao baada ya kupangwa na Simba SC kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

“Simba SC ni timu nzuri na inayosafiri sana, ina uzoefu wa kutosha na ni timu kubwa sana Tanzania,” amesema Johnson akiwaambia wanahabari.

“Kuikabili Simba SC nyumbani kwao ni ngumu sana, sijui ni watu elfu ngapi watakuwepo uwanjani kuwashuhudia.

“Lakini mara ya mwisho nilikuwa pale na Al Ahly kulikuwa na mashabiki 30,000 hadi 40,000 uwanjani, hivyo utakuwa mchezo mgumu sana kwa Orlando Pirates nchini Tanzania na wanatakiwa kujiandaa vilivyo kuwakabili,” ameongeza kocha huyo.

Cavin Johnson alipokua kibaruani Al Ahly

Simba iliichapa Al Ahly bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ikiwa chini ya Kocha Mkuu wa sasa Raia wa Afrika Kusini Pitso Mosimane akisaidiwa na Johnson kwenye mchezo wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Februari 23, 2021.

Lilikuwa ni bao la raia wa Msumbiji, Luis Miquissone, ambalo lilimpa moja kwa moja tiketi ya kusajiliwa na klabu hiyo ambao ni Mabingwa wa Afrika kwa sasa.

Ulikuwa ni msimu ambao Simba iliongoza kundi A, ikiwa na alama 13, ikifuatia na Al Ahly ambayo ilimaliza ikiwa na alama 11, AS Vita Club ya Jamhuri ya Kimokrasi ya Congo alama saba na Al Merrikh ya Sudan iliyomaliza na alama mbili.

Johnson mwenye umri wa miaka 63 raia wa Afrika Kusini, amewahi pia kuwa Kocha Mkuu wa timu za Platinum Stars (mara mbili), SuperSport United, AmaZulu na Black Leopards (zote za Afrika Kusini).

Oktoba mwaka 2020, aliteuliwa kwa kocha msaidizi wa Al Ahly chini ya Pitso Mosimane ambako alidumu hadi mwaka 2021.

Simba SC itaanzia nyumbani Jumapili (Aprili 17), kabla ya kusafiri kwenda Houghton Jijini Johannesburg kwa mchezo wa marudiano Jumapili (Aprili 24.)

Harsi Said: Tutachukua Ligi Kuu, ASFC
Declan Rice kuvunja rekodi Old Trafford