Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC, Mulamu Nghambi amesema wameuweka kiporo mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans ambao umepangwa kucheza April 30 Uwanja wa Benjamin Mkapa, ili kuhakikisha wanapambana kuiwezesha timu yao kufuzu Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC inakabiliwa na mchezo wa Mkondo wa Pili, Hatau ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika utakaochezwa Jumapili (April 24), katika Uwanja wa Orlando mjini Johannesburg.
Mulamu amesema kwa sasa Simba SC haiwezi kutoa kipaumbele kwenye mchezo dhidi ya Young Africans, kutokana na kazi kubwa iliyo mbele yao ya kuhakikisha wanapambana na kupata matokeo mazuri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, Hatua ya Robo Fainali.
“Hatuwezi kufikiria mchezo wa mbele zaidi kuliko uliopo karibu, sisi tumejipanga kuhakikisha malengo yetu tuliyojiwekea ni kuwatoa wapinzani wetu na kufuzu hatua inayofuata,” amesema Mulamu na kuongeza;
“Baada ya hapo sasa tutaangalia kilichopo mbele yetu na ni maandalizi kwa ajili ya hao watani zetu huku tukiamini licha ya kutopoteza ila mchezo wao wa kwanza kufungwa msimu huu watafungwa na Simba.” Amesema
Jumapili (April 17) Simba SC ilishinda mchezo wake wa Mkondo wa kwanza Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0, ama kusaka ushindi zaidi katika mchezo wa Mkondo wa pili ugenini Afrika Kusini siku ya Jumapili (April 24), ili kupata tiketi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa upande wa Orlando Pirates italazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuelendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.