Kikosi cha Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, kimeanza kufanya mazoezi nchini Nigeria ikiwa ni sehemu ya kukamilisha Program ya maandalizi ya mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Palteau United.

Msafara wa Simba SC wenye watu 40 uliwasili jana mchana mjini Abuja, Nigeria ukitokea Addis Ababa Ethiopia walipopitia, baada ya kuondoka nchini Jumatatu jioni (Novemba 23), Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wachezaji wa Simba walianza kufanya mazoezi ya Gym kwa ajili ya kuiweka miili yao sawa, na kisha wameendelea na mazoezi ya uwanjani chini ya kocha Sven Vandenbroeck akisaidiana na kocha mzawa Suleyman Matola.

Wakati mipango ya maandalizi ya mwisho ikiendelea, taarifa kutoka nchini Nigeria zinaeleza kuwa, benchi la ufundi la Simba SC limezinasa siri zote zinazowahusu wapinzani wao Plateau United, ikiwemo staa wao matata.

Simba SC wamepata siri hizo ikiwa ni siku chache kabla ya kucheza na Plateau United kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali, huku wakielezwa, Junior Salomon raia wa Benin ndiye mtu wa kumchunga kutokana na madhara aliyokuwa nayo.

 “Kwa sasa tuna siri zote za wapinzani wetu Plateau United kabla ya kucheza nao, ikiwemo ya mtu hatari ambaye tunatakiwa kumuangalia zaidi.

“Huyo ni Junior Salomon raia wa Benin ambaye ndiye mtu muhimu kikosini hapo, hivyo lazima achungwe kwa dakika zote.

“Lakini pia wachezaji wanatakiwa kwenda kushambulia na kupata ushindi kwenye mechi hii na kumaliza kila kitu kabla ya kurudi Dar kurudiana nao,” imeeleza taarifa hiyo.

Simba SC itacheza mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United Jumapili hii (Novemba 29), Uwanja wa New Jos saa kumi jioni (sawa na saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki).

Watumishi 8 wasimamishwa kazi kwa kukosa maadili
ATCL yafunguka kuhusu mapokezi ya Bombardier nyingine

Comments

comments