Uongozi wa Simba SC umeamua kujilipua mapema kwa kuandaa kamati maalum ya watu 10 watakaohakikisha wanaiwezesha klabu hiyo kuvuna pointi tatu nchini Morocco dhidi ya Wydad Casablanca, ambapo tayari baadhi ya wajumbe wametangulia Marrakech kuandaa mazingira.
Simba SC ambao wameondoka jana Jumanne (Desemba 05) nchini kueleka Morocco wapo nafasi ya tatu kwenye Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ikiwa na pointi mbili, huku Wydad wao wakiburuza mkia baada ya kupoteza michezo yote miwili, katika Kundi hilo linalozijumuisha timu za Jwaneng Gallaxy ya Botswana, Wydad ya Morocco na AseC Mimosas ya Ivory Coast.
Chanzo cha kutoka Simba SC kimeeleza kuwa, Viongozi wameamua kuiwekea mkazo mechi hiyo kwa kuichukulia kama fainali maana wanajua kuwa Wydad pia anazitaka pointi tatu jambo ambalo sasa limewafanya kuandaa kamati maalumu ya ushindi.
“Tunahitaji sana kuvuna pointi tatu kwenye mchezo wetu na Wydad jambo ambalo limetufanya kuongeza viongozi maalum ili waweze kutuhakikishia hilo, hivyo tayari kuna watano kati yao wapo safarini kwa ajili ya kuandaa mazingira rafiki ya mchezo huo,” kilisema chanzo hicho.
Simba SC kupitia kwa Meneja Habari na Mawasiliano wao, Ahmed Ally amesema: “Hatuna namna zaidi ya kuhitaji pointi dhidi ya Wydad, kwani tunajua wazi ili malengo yetu yafikie ni lazima tupate pointi tatu nyumbani na ugenini au nne ili kujisogeza kwenye kundi letu.”