Wekundu wa Msimbazi Simba wamebanwa mbavu kwa kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Al Masry katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa kombe la Shirikisho Afrika uliounguruma jijini Dar es salaam kuanzia mishale ya saa kumi na mbili jioni.
Simba ilipata bao la kwanza dakika ya tisa kwa mkwaju wa penati uliopigwa na mshambuliaji John Bocco, ambapo hata hivyo halikudumu baada ya Ahmed Gomaa kusawazisha dakika ya 11.
Al Masry walipata bao la pili kwa mkwaju wa penati dakika ya 25 kupitia kwa Ahmed Abdulraof kufuatia James Kotei kuunawa mpira katika eneo la hatari, lakini mshambuliaji kutoka nchini Uganda Emmanuel Okwi aliisawazishia Simba dakika ya 74 kwa penati pia.
Hata hivyo mchezo huo uliingia dosari baada ya umeme kukatika uwanjani dakika ya 80 na kusimama, kabla ya kuendelea tena lakini matokeo hayakubadilika.
Hii ina maana kuwa, Simba itatakiwa kupata ushindi wowote au sare inayoanzia mabao matatu katika mchezo wa mkondo wa pili, ili kufanikisha mpango wa kusonga mbele katika michuano ya kombe la shirikisho.
Mchezo wa mkondo wa pili unaotarajiwa kuwa mgumu kwa Simba, umepangwa kuchezwa nchini Misri, Machi 16.