Uongozi wa Simba SC, umeweka wazi kwamba, unapitia kwenye kipindi kigumu baada ya kutoka kupoteza mchezo dhidi ya Young Africans kwa idadi kubwa ya mabao.

Simba SC katika mchezo uliopita wa ligi kuu dhidi ya Young Africans, walipoteza kwa mabao 5-1, jambo ambalo limepelekea kumfukuza kocha wao, Roberto Oliviera ‘Robertinho’.

Simba leo Alhamisi (Novemba 09) inatarajiwa kukipiga dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmedy Ally, amesema kwa sasa hawatakiwi kupoteza mchezo unaofuata kulingana na matokeo waliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Young Africans.

Kiongozi huyo aliongeza kwamba, ambacho wanatakiwa kukifanya kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda ili mambo yasiwe mabaya zaidi.

“Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Young Africans tena kwa idadi kubwa ya mabao, lazima vitu vingi vitokee ndani ya timu kutokana na ukubwa wa timu yetu na mambo mengine mengi, hivyo Wanasimba wanatakiwa wasitukatie tamaa.

“Tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda katika mchezo wetu dhidi ya Namungo FC kwa sababu naamini kama tutapoteza mchezo huo basi mambo yatazidi kuwa magumu kwa upande wetu,” amesema Ally.

Kibu Denis: Siamini katika kubebwa, ninapambana
Kasi upimaji wa Ukimwi kwa Vitepe yaongezeka Mara