Uongozi wa Simba SC umethibitisha kuhamishwa kwa mchezo wao wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Ihefu FC kutoka Uwanja wa Uhuru na kupelekwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Simba SC ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo uliopangwa kuchezwa kesho Ijumaa (April 07), awali ilipanga kuutumia Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 10:00.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema Uwanja wa Uhuru kesho Ijumaa (April 07) utakuwa na matumizi mengine na kulazimisha waandaaji wa michuano ya ASFC, Shirikisho la Soka ‘TFF kufanya mabadiliko hayo.
Ahmed amesema sababu kubwa za mabadiliko hayo ni kutokana na Uwanja wa Uhuru uliopangiwa kutumika kwa shughuli za mashindano makubwa ya usomaji wa Quran tukufu, ambapo kesho utakuwa ukiandaliwa kwa ajili ya Mashindano hayo yatakayofanyika Jumapili (April 09).
“Tumepokea mabadiliko hayo kwa sababu Uwanja wa Uhuru siku hiyo ya Ijumaa utatumika kwa ajili ya mashindano makubwa ya usomaji wa Quran tukufu hivyo tukaona ni vyema tuhamishie mchezo wetu Chamazi,” amesema Ahmed.
Mshindi wa jumla katika mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Ihefu FC atakutana na Azam FC katika hatua ya Nusu Fainali baada ya kikosi hicho cha matajiri wa jiji la Dar es Salaam kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Mtibwa Sugar Jumatatu (April 03), Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Simba SC ilifika hatua hiyo baada ya kushinda mabao 4-0 dhidi ya African Sports huku Ihefu FC ikishinda 2-0 dhidi ya Pan Africans katika Raundi ya 16 Bora.
Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu Bara timu hizo zilipokutana Simba ilishinda bao 1-0 Novemba 12, mwaka jana lililofungwa na Pape Sakho.
Baada hapo timu hizo zitakutana tena Aprili 10 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Highland Estate Mbeya.
Singida Big Stars ndio timu ya kwanza hadi sasa kutangulia nusu fainali baada ya kuifunga Mbeya City kwa mabao 4-1 kwenye mechi ya Robo Fainali.