Bao la Gerard Mdamu limeifanya Mwadui FC kuwa timu ya kwanza kuwafunga mabingwa watetezi Tanzania bara msimu huu Simba SC kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Mwadui ikicheza kwa kujiamini ilipata bao hilo katika dakika 33, lililofungwa na Mdamu akiunganisha kwa kichwa krosi ya beki wa kushoto Khalfan Mbaruku.
Katika mchezo huo kocha wa Simba, Patrick Aussems alimwazisha mshambuliaji mmoja Meddie Kagere huku akijaza viungo wengi.
Mwadui ilikuwa ikicheza kwa kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo kama wangekuwa makini wangeweza kufunga mabao zaidi.
Washambuliji Mdamu na Ludovic Venance walikuwa mwiba kwa ngome ya ulinzi ya Simba iliyokuwa chini ya Erasto Nyoni na Tairone Santos.
Mwadui walikuwa wazuri katika eneo la katikati lililokuwa linachezwa na Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’ pamoja na Raphael Obina na kuwafanya viungo wa Simba, Mzamiru Yassin na Clatous Chama kuhaha katika eneo hilo.
Uwezo wa viungo wa Mwadui kucheza katika uwanja wa CCM Kambarage, ulionekana kuwa tofauti na kwa upande wa Simba ambao walikuwa wanashindwa kuumiliki mpira ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, lakini hali ilibadilika kipindi cha pili.
Matokeo haya yanaifanya Simba ipoteze kwa mara ya kwanza msimu huu lakini ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na alama zake 18.
Matokeo ya michezo mingine Lipuli 2-1 Polisi Tanzania, Singida United 1-2 JKT Tanzania, Kagera Sugar 2-0 Namungo, Ruvu Shooting 1-0 KMC, Mtibwa Sugar 2-1 Coastal Union.