Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amemtaka Mdau wa Klabu hiyo Mbunge Hamis Kigwangala kufuata taratibu za kuwasilisha ushauri ama malalamiko yake, na sio kupayuka na kuandika katika mitandao ya kijamii.
Kigwangwala ni sehemu ya wadau wa Simba SC walioonesha kuchukizwa na matokeo ya klabu hiyo msimu huu, sambamba na kupoteza mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Try Again amesema Kigwangala ana nafasi kubwa ya kuwasilisha maoni na malalamiko yake kwa njia sahihi, huku akimtaka kumtumia Mjumbe wa Bodi Rashid Shangazi ambaye ni Mbunge.
Amesema anaamini Kigwangwala ana nafasi ya kuonana na Shangazi na kusema dukuduku lake, na sio kutumia njia ambazo zinamvunjia heshima kama Muwakilishi wa Wananchi.
“Tumemsikia Dk Hamis Kigwangalla. Tumepokea ushauri wake, lakini ni vizuri kusema mapema, kwa nini anasubiri kusema? Pale bungeni kuna Rashid Shangazi ni mjumbe wa bodi angeweza kuwasilisha ushauri wake.”
“Nawashauri viongozi wenzangu, ni vizuri kushauri, lakini tutumie njia bora. Kwa nini tulipofanya vizuri nyuma hawakusema? Haipendezi wajumbe wa bodi wana nafasi ya kushauri ndani, lakini wanatoka wanakwenda kuzungumza huko nje. Si jambo jema.” Amesema Try Again
Katika hatua nyingine Try Again amezungumzia mipango na mikakati ya kufanya marekebisho na maboresho kwenye kikosi cha Simba SC, baada ya kuanza na Kocha Mkuu Franco Pablo Martin
Try Again anasema; “Tunarudi kwa kishindo, tunarudi kwa kishindo. Nimezungumza na mwekezaji wetu MO Dewji kuwa atasajili (wachezaji).
“Tutawekeza kwenye miundombinu, kikubwa tunaomba wapenzi wa Simba tumpe ushirikiano, lakini tunawaahidi tutarudi kwa kishindo.
“Sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kikosi, tunasajili vizuri, tutabaki na wachezaji wazuri, kuna wengine umri umekwenda na viwango vimeshuka, lakini hatutawaacha vibaya…Tunawashukuru sana wachezaji na benchi la ufundi.