Mtendaji mkuu wa Klabu ya Simba, Senzo Mazingiza amedai kuwa, pamoja na makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Young Africans, Fredrick Mwakalebela kuomba msamaha kuhusu suala la Clatous Chama, bado ameendelea kufanya makosa yale yale.

Senzo amedai katika maelezo Mwakalebela aliyoyatoa jana jioni kwa kudhihirisha hakufanya mazungumzo na Chama, bado aliendelea kuizushia klabu ya Simba kwa kusema iliwahi kufanya mazungumzo na kiungo wa Young Africans Papy Kabamba Tshishimbi ambaye bado ana mkataba.

Kiongozi huyo amesema Mwakalebela anapaswa authibitishie umma kauli yake kama kweli uongozi wa Simba SC ulishawahi kufanya mazungumzo ya kumsajili, Papy Tshishimbi siku za karibuni.

“Bado kuna tatizo kwa huyu kiongozi wa Young Africans, ametutuhumu kufanya mazungumzo na mchezaji wao, jambo ambalo sio kweli, anapaswa kuthibitisha kwa ushahidi kama tuliwahi kufanya hivyo.”

“Haiwezekani anaomba radhi kwa kosa la Clatous Chama, halafu  anaendelea kufanya makosa ya kututuhumu kufanya jambo ambalo halikuwahi kufanywa na viongozi wa Simba SC, zaidi ya kuandikwa kwenye mitandao ya kijamii.”

“Simba SC ina heshima yake na itaendelea kujilindia heshima yake, haitochafuliwa kirahisi kama hatua zilizochukuliwa na kiongozi huyo wa Young Africans.”

Katika maelezo yaliyotolewa jana na Mwakalebela alipokua akiomba radhi kwa kosa la kudanganya kuhusu mpango wa kuzungumza na Chama alisema: “Hapa katikati tumekua na mazungumzo ya utani utani kati yetu na wenzetu Simba SC, ukiangalia hata kwenye mitandao ya kijamii wakielezea kuchukua wachezaji wetu, hasa suala la Tshishimbi lililokua limepita nikaona na mimi niseme jambo.”

Kabla ya kuomba radhi kwa kiongozi huyo wa Young Africans, uongozi wa Simba SC ulitangaza kuichukulia hatua klabu hiyo kwa kuwasilisha mashtaka TFF na FIFA kwa kosa la kufanya mazungumzo na Clatous Chama, ili hali ikifahamika bado ana mkataba.

Hata hivyo hadi sasa uongozi wa Simba SC haujatoa kauli yoyote ya kukubali ombi la msamaha ulioombwa na Mwakalebela ama kusitisha taratibu za kuwasilisha mashtaka yao TFF na FIFA.

Magufuli atuma rambirambi vifo ajali ya Mkuranga
Bifu zito FC Barcelona