Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC imevunja mkataba na Patrick Aussems kama kocha mkuu wa timu hiyo kuanzia leo Novemba 30, 2019.
Taarifa ya kuvunjwa kwa mkataba huo imetolewa leo na uongozi wa Simba kupitia mitandao yake rasmi ya kijamii ikiwa ni dakika chache baada ya kocha huyo pia kutoa taarifa kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii kuwa bodi hiyo imeamua yeye asiendelee kuwa kocha wa timu hiyo.
SABABU ZA KUACHANA NA AUSSEMS
1. Kushindwa kufikia malengo
Kwa mujibu wa taarifa ya Simba, bodi imefikia uamuzi huo baada ya Aussems kushindwa kutekeleza majukumu kwa viwango na malengo ambayo walikubaliana kwenye mkataba wa ajira ikiwa ni pamoja na kushindwa kufika katika hatua ya makundi kwenye michuano ya Mabingwa Afrika 2019/20.
“Pamoja na jitihada za dhati za bodi kumpa ushirikiano Aussems hata baada ya kutolewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, bado kocha ameendelea kuisimamia timu bila kujali malengo ya Simba ya kujenga timu yenye ari ya mafanikio, nidhamu, na ushindani kwenye michuano ya ndani na nje ya nChi”, imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
2. Kuondoka kazini bila ruhusa
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu Senzo Mbatha imeendelea kusema kuwa bodi haikuridhika na maelezo ya kocha huyo ilipomuita katika kikao cha nidhamu Novemba 28, 2019 juu ya kuondoka kwake kwenye kituo cha kazi bila ruhusa ya uongozi na kwamba alikataa kuiambia kamati sehemu alipokuwa na sababu za kwenda bila ruhusa.
Bodi hiyo imemteua Kocha Msaidizi Denis Kitambi kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu wakati mchakato wa kutafuta kocha mbadala ukianza mara moja.

Juma Mwambusi aachia ngazi Mbeya City FC
Ajinyonga baada ya kumkosa mkewe kitandani