Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amewasilisha mapendekezo kwa Uongozi wa klabu hiyo ya kutaka aongezewe nguvu katika Benchi la Ufundi ya makocha wengine wawili watakaofanya kazi kwenye maeneo mbalimbali.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania, ameutaka Uongozi wa Simba SC kumuajiri kocha msaidizi mwingine, huku akipendekeza kuletewa Mkurugenzi wa Michezo wa kuja kuongeza nguvu kikosini pamoja timu za vijana na ile ya wanawake ya Simba Queens.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa katika eneo la Mkurugenzi wa Michezo, Pablo amempendekeza, Arno Buitenweg aliyewahi kufanya kazi katika timu mbalimbali kwa nafasi tofauti.
Mtaalam huyo aliyebobea kwenye soka la vijana anatajwa ni fundi wa soka la pasi nyingi maarufu kule Hispania kama tiki-taka huku akifundisha timu kutoka nchini kwao Uholanzi, Hispania ikiwamo Real Mallorca pamoja na Uarabuni.
Taarifa hiyo inaeleza Pablo amemtaka Arno kwa ajili ya kushauri na kushirikiana katika masuala ya kiufundi kwa timu ya wakubwa pamoja na kuwekeza nguvu Simba Queens na ile ya vijana ili kuzalisha wachezaji bora watakaopata nafasi katika timu ya wakubwa au kuuzwa.
Inaelezwa mabosi wa Simba baada ya kukubaliana na ombi hilo la kumleta Arno, lakini waliamua kwanza kuzungumza naye ikiwemo kumtumia majukumu atakayotakiwa kuyafanya akija nchini na kukubaliana masilahi watakayomlipa.
Japo haijawekwa wazi walipofikia, lakini kama Arno atakubaliana na majukumu hayo pamoja na maslahi atakayopata Simba SC atawasili nchini muda wowote ndani ya juma hili ili kusaini mkataba kabla ya kuanza kazi Machi Mosi 2022.
Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya Ajax Amsterdam na Al Arabi SC ya Qatar na kufanya kazi na kituo cha kimataifa cha kukuza na kuendeleza soka la vijana cha Aspire Academy, ana leseni za AFC Pro na UEFA Leseni A akifanya kazi kama kocha na Mkurugenzi wa Ufundi kwa baadhi ya timu barani Ulaya na Asia.
Arno aliwahi kuwa mkufunzi wa makocha katika Shirikisho la Soka visiwa vya Balearic kisha akaajiriwa kama kocha wa Al-Arabi na baadae kuwa Kocha wa timu ya taifa ya Qatar.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alipoulizwa kuhusu jambo hilo alisema uongozi upo tayari kuwapatia kila wanachohitaji benchi la ufundi ili kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo ya klabu.
“Simba tuna malengo ya muda mrefu na kufanya vizuri katika kila mashindano tutakayokuwepo, hivyo tumejipanga kuboresha katika maeneo yote ikiwemo kusikiliza benchi la ufundi linahitaji vitu gani,” alisema Barbara mwenye kiu kubwa msimu huu kuona Simba inafika mbali katika michuano ya Shirikisho Afrika ambayo itaendelea tena mwishoni m wa juma hili kwa Mnyama kucheza dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Kuelekea kwenye mchezo huo Kocha Pablo anatarajiwa kuanza maandalizi mara baada ya kuwasili nchini Morocco baadae leo Jumanne (Februari 22).
Hata hvyo katika maandalizi hayo Kocha Pablo anatarajiwa kumtumia sana Clatous Chama aliyesafiri naye, ili kuisasambua RS Berkane nyumbani kwao katika mchezo wa Februari 27, siku ya Jumapili.
Chanzo: Mwanaspoti