Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara umeliandikia Barua Shirikisho la soka Barani Afrika ya kuomba kuongezewa Mashabiki watakaoshuhudia mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho dhidi ya USGN ya Niger.

Simba SC itakua mwenyeji wa USGN Jumapili (April 03) Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku CAF ikiruhusu mashabiki 35,000 kushuhudia mchezo huo wakiwa uwanjani.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema wameandika barua CAF kuomba kuongezewa mashabiki wengine 10,000 ili kufikia idadi ya Mashabiki 45,000.

Ahmed amesema wamewasilisha ombi hilo, wakiamini nguvu ya timu yao kufanya vizuri ipo kwa mashabiki wa Simba SC ambao wamekua na msaada mkubwa hasa timu yao inapokua kwenye majukumu ya Kimataifa.

Amesema bado wanasubiri majibu kutoka CAF, na endapo watakubaliwa ama kukataliwa watawafahamisha Wanasimba kupitia vyombo vya habari na kurasa zao za mitandao ya kijamii.

“Tunatambua umuhimu wa hamasa hasa kukiwa na mashabiki wengi, watasaidia kuhamasisha wachezaji kuonesha bidii uwanjani na kupigania ushindi ambao utatuvusha kwenda hatua nyingine, tunasubiri majibu tunaamini tutakubaliwa.” Amesema Ahmed.

Simba SC itahitaji kushinda mchezo dhidi ya USGN ili kujihakikishia kucheza Robo Fainali Kombe la Shirikisho kwa kufikisha alama 10, huku mshiriki mwingine wa hatua hiyo kutoka Kundi D akitarajiwa kutoka kwenye mchezo kati ya RS Berkane itakayokua nyumbani Morocco ikicheza dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast siku hiyo ya April 03.

Msimamo wa Kundi D unaonyesha ASEC Mimosas ya Ivory Coast inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane ya Morocco yenye alama 07 sawa na Simba SC ya Tanzania, huku USGN ikiburuza mkia kwa kufikisha alama 05.

Rais Dkt Mwinyi ahimiza wana CCM kujibu hoja kwa vitendo
Kim Poulsen kuongezea makali safu ya ulinzi