Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC umewaomba radhi Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kufuatia matokeo ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City jana Jumatatu (Januari 17).
Simba SC ilikua ugenini Jijini Mbeya katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine na ilikubali kipigi cho cha kwanza katika Ligi Kuu msimu huu 2021/22.
Simba SC imetoa neno la kuomba radhi kwa Mashabiki na Wanachama wake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ambapo inaamini neno hilo litafika kwa wakati na litawafikia wengi.
“Tumehuzunishwa wote kwa matokeo ya jana. Safari ya ubingwa bado ni ndefu na malengo yetu ni kutetea ubingwa.”
Kwa matokeo hayo Simba SC inaendelea kuwa na alama 24 zinazoiweka nafasi ya pili, baada ya kucheza michezo 11, huku Mbeya City ikifikisha alama 19 na kukwea hadi nafasi ya tatu.
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 32, baada ya kushuka dimbani mara 12.