Meneja wa Habari na Mawasiliani wa Simba SC, Ahmed Ally amesema wamejipanga kikamilifu kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya dhidi ya Mabingwa wa Angola Premeiro De Agosto.
Simba SC itaanzia ugenini Angola Jumapili (Oktoba 09) katika Uwanja wa França Ndalu mjini Luanda, huku kikosi kikiratajiwa kusafiri kwa ndege maalum ya kukodi Jumamosi (Oktoba 08).
Ahmed amesema kwa kuzingatia umuhimu wa mchezo huo, Uongozi tayari umeshakamilisha taratibu zote za maandalizi watakapokua nchini Angola, kwa kutuma watu mjini Luanda ili kuweka mambo sawa kabla ya kikosi hakijawasili.
“Ni kweli tayari kuna watu walienda Angola tangu juma lililopita kwa ajili ya kuweka mambo yote sawa, hivyo hatuna shaka ya lolote kutokea huko,”
“Tunamshukuru Mungu, hadi sasa tumeshajua baadhi ya mbinu za wapinzani wetu na kwamba tunatengemea hadi kikosi kinapofika nchini Angola, hakitakumbana na changamoto yoyote ya kuhujumiwa, maana watu wetu wa kuandaa mazingira wameshaingia huko na kushughulikia mambo yote muhimu.”
“Tunashukuru sana kufahamu baadhi ya mambo ambayo yatalisaidia zaidi benchi la ufundi katika mchezo huo, ambao kwa kiasi fulani mazingira yapo sawa na kwamba tutacheza bila presha kwani tumeshategua mitego yao mingi waliyokuwa wamejiandaa nayo,” amesema Ahmed Ally
Baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza kupigwa Angola mwishoni mwa juma hili, Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Pili dhidi ya Premeiro De Agosto, utakaopigwa Jumapili (Oktoba 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.