Simba SC imepoteza Mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Haras Al Hodoud mjini Cairo-Misri, uliopigwa leo Jumatano (Julai 27) majira ya jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Simba SC iliyoweka Kambi ya Kujiandaa na Msimu mpya wa 2022/23 mjini Ismailia-Misri, ilicheza mchezo huo kama sehemu ya maandalizi yake, ukiwa mchezo watatu wa Kirafiki.
Ikicheza chini ya uangalizi wa Benchi Jipya ya Ufundi linaloongozwa Kocha Zoran Maki, timu ya Simba SC imepoteza kwa kufungwa 2-0.
Matokeo hayo yanakua mabaya kwa Simba SC, tangu walipoanza Kambi nchini Misri, kwani waliwahi kupata matokeo ya ushindi wa 6-0 dhidi ya Abou Hamad, yakitanguliwa matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Ismailia FC.
Hata Hivyo Idara ya Habari na Mawasiliano inayoongozwa na Meneja Ahmed Ally imeeleza kuwa, michezo hiyo inaendelea kumsaidia Kocha Zoran na Jopo lake kutatua baadhi ya changamoto zilizopo kwenye kikosi chao.
Simba SC leo imefikisha siku yaa 12 tangu ilipoanza Kambi mjini Ismailia-Misri, huku ikitarajia kurejea Dar es salaam Tanzania mwanzoni mwa mwezi Agosti 2022.
Itakaporejea Dar es salaam, Simba SC itacheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki utakaohitimisha sherehe za Simba Day, mnamo Agosti 08-2022.
Agosti 13 Simba SC itacheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Mtani wake Young Africans, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.