Uongozi wa Simba SC umepotezea ishu ya usajili wa Kiungo wa Azam FC Sospeter Bajana, kwa kusema bado mapema kuzungumzia suala hilo, japo umekiri kuanza mchakato wa usajili kwa ajili ya msimu ujao 2023/24.
Simba SC imeanza kuhusushwa na usajili wa baadhi ya wachezaji wa ndani na nje ya Tanzania, huku Bajana akitajwa kuwa kipaumbele kwa wachezaji wanaowindwa klabuni hapo kwa sasa.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu hiyo Ahmed Ally amesema wako kwenye mawindo makali na kama kocha wao Robertinho (Oliviera) atamtaka mchezaji huyo watakaa meza moja kumsajili.
“Sio Bajana tu, mchezaji yeyote ambaye kocha wetu atapendekeza tutakaa naye kwa ajili ya mazungumzo na kama ana mkataba na klabu nyingine basi tutakaa na klabu hiyo kuangalia namna ya kumsa-jili, Simba ni timu kubwa hivyo wachezaji wengi wanatamani siku moja kuichezea,” amesema Ahmed
Hata hivyo, imefahamika kuwa Simba SC imeshaanza mazungumzo na Bajana kuangalia uwezekano wa kumsajili hasa baada ya mkataba wa nyota huyo kueleka ukingoni.
Kwa upande wa Sospeter Bajana amekiri kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba SC kwa ajili ya kumsajili.
“Sasa ni mapema kusema msimu ujao nitacheza wapi, kwa sababu mkataba wangu kwa sasa upo ukiongoni, nafanya mazungumzo na Azam FC kwa ajili ya mkataba mpya lakini Simba SC wameonyesha nia ya kunisajili, soka ni kazi yangu naangalia maslahi zaidi kwa sababu nina familia ambayo inanitegemea, hivyo kubaki Azam FC au kwenda Simba SC ni suala la nani mwenye ofa nzuri,” amesema Bajana