Uongozi wa Simba SC, umeweka wazi kuwa malengo yao makubwa kwenye mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu ni kukomba pointi tatu kila wanaposhuka uwanjani ili kuendeleza kasi waliyoanza nayo msimu wa 2023/24.
Chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira, Simba SC imecheza mechi tano ambazo ni dakika 450 ikikomba pointi 15, inashika nafasi ya kwanza na bado haijapoteza mchezo.
Kete yake ya tano ilikuwa ugenini iliposhuhudia ubao wa Uwanja wa Liti ukisoma Singida Fountain Gate 1-2 Simba SC, bao la ushindi kwa Simba lilifungwa na Moses Phiri aliyetokea benchi.
Simba SC imebakiwa na mechi 25 sawa na dakika 2,250 zenye pointi 75 kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Ahmed Ally, Meneja wa ldara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, amesema baada ya kukamilisha mechi tano wanahitaji kuendeleza kasi hiyo kwenye mechi zilizobaki.
“Hizi mechi tano hesabu zimekamilika tumetulia na pointi zetu 15, tunaongoza ligi. Tuna safari ndefu bado ikiwa ni mechi 25 zilizobaki nazo tunahitaji kushinda kwani furaha ya Wanasimba ni kupata pointi tatu.
“Wale wanaotaka ‘show game’ kwa sasa hatuwezi kuwaahidi kwa kuwa uhitaji wetu mkubwa ni pointi tatu. Kazi bado ni ngumu, hilo lipo wazi, wapinzani wetu wanaonesha uwezo mkubwa, lakini bado hatujamaliza kuwa kwenye mapambano,” amesema Ahmed Ally