Uongozi wa Simba SC umeshangazwa na maneno yanayoendelea mitandaoni kwa kuihusisha klabu hiyo kuhofia kukutana na Young Africans kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Simba SC imeshakutana na Young Africans mara mbili kwenye Ligi msimu huu 2021/22, huku miamba hiyo ikimaliza dakika 180 pasina kufungana.
Taarifa kutoka kwenye Mitandao ya Kijamii zinaeleza kuwa Simba SC inahofia kukutana na Mtani wake kwenye hatua ya Nusu Fainali, na huenda ikautumia mchezo wa Robo Fainali ya ‘ASFC’ dhidi ya Pamba FC kujiondoa kwa makusudi ili kuepuka kadhia ya kukutana na Young Africans.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema taarifa hizo ni za mitandaoni na haziwashtui, lakini kikubwa kwao ni kuhakikisha wanashinda dhidi ya Pamba FC ili kutinga Nusu Fainali ya ‘ASFC’.
“Sisi huyo Pamba FC tunaona kama anatuchelewesha, anatuchelewesha pakubwa, tunataka tumnyoa Pamba FC mapema ili aendelee na Ligi Daraja la Kwanza, kisha tutinge Nusu Fainali ili kuthibitisha tunawahitaji tena hao wanaosemwa mitandaoni eti tumepanga kuwakimbia.”
“Simba SC tunaitaka kweli kweli hiyo Nusu Fainali, ndio Mechi iliyosalia kumaliza ubishi na hawa jamaa msimu huu, kwa sababu tunahitaji kutabasamu kwenye mioyo yetu, tuna majonzi ya kutolewa Kombe la Shirikisho na kutoka sare na hawa jamaa Jumamosi.” amesema Ahmed Ally
Tayari Young Africans imeshatangulia Nusu Fainali, baada ya kuifunga Gaita Gold FC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati, na itacheza na mshindi wa mchezo wa Simba SC dhidi ya Pamba FC.