Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC umeshauriwa kufanya usajili wa Kiungo Mchezeshaji ili kuondokana na tatizo linalokisumbua kikosi chao katika kipindi hiki cha msimu wa 2021/22.
Simba SC imeanza kwa mwenendo mbaya msimu huu licha ya kutopoteza mchezo wowote hadi sasa, lakini imejikusanyia alama 11 katika michezo mitano.
Ushauri kwa viongozi wa Simba SC umetolewa na aliyekuwa Kocha wa Viungo wa klabu hiyo Adel Zrane ambaye aliondolewa katika nafasi yake mwishoni mwa Mwezi Oktoba sambamba na Kocha wa Makipa kutoka Brazil Milton Nienov.
Zrane amesema tatizo kubwa linaloisumbua Simba SC kwa sasa ni kiungo Mchezeshaji, hasa baada ya kuondoka kwa Clatous Chotta Chama aliyejiunga na RS Berkane ya Morocco.
“Katika kipindi cha dirisha la usajili la mwezi Agosti mwaka huu, Simba ilifanya usajili mzuri sana lakini changamoto kubwa ilikuwa ni ishu ya kuzoea mazingira na ndiyo maana kumekuwa na hali ya kusuasua.”
“Hivyo kwa upande wangu naamini wakati Simba wakiendelea kuwavumilia nyota wapya, wanapaswa kusajili angalau kiungo mmoja mchezeshaji atakayekuwa na uwezo mkubwa kwa ajili ya kuongeza nguvu zaidi.” amesema Zrane
Hata hivyo Simba SC ni sehemu ya klabu ambazo zinatajwa kufanya usajili wa baadhi ya wachezaji wakati wa dirisha dogo la usajili ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15 mwaka huu.