Kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, imeelezwa kumewaamsha viongozi wa Tanzania Prisons wakianza kukosa imani na kocha mkuu wa kikosi hicho, Fred Felix ‘Minziro’.
Prisons ilianza msimu kwa suluhu mbele ya Singida Fountain Gate kabla ya kuchapwa mabao 3-1 na Azam na Tabora United kila moja, jambo lililowafanya mabosi wa klabu hiyo kuanza kuingiwa na wasiwasi juu ya kiwango cha timu.
Taarifa za kuaminika zinaeleza endapo matokeo mabaya yataendelea basi huenda muda wowote Minziro atafungashiwa virago, huku mechi ijayo dhidi ya Simba SC itakayopigwa Oktoba 5 ikiwa kipimo cha kutetea kibarua hicho.
“Ni kocha mzuri, ila kuna mambo hayapo sawa, tunahofia linaweza kutuletea shida huko mbele, japo bado tunaendelea kulifuatilia,” kilisema chanzo chetu, lakini Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Jackson Mwafulango alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, amesema hizo ni tetesi tu zinazozungumzwa ila wao kama viongozi wana imani kubwa na kocha na hawawezi kufanya jambo hilo.
“Viongozi wetu ni watu wa soka, ni jambo la kushangaza kumpima kocha katika michezo mitatu ya awali, sisi tuna imani naye. Nikuhakikishie tu ndugu yangu tutaendelea kumpa sapoti yetu kama kawaida,” amesema.