Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umefurahia ujio wa Msaada wa Video kwa Mwamuzi (VAR) itakayotumika kwa mara ya kwanza katika hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Afrika.

Furaha hiyo kwa Uongozi wa Simba SC imeibuka, ikiwa ni siku chache tangu Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kutangaza kutumika kwa Teknolojia ya VAR, ambayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam itatumika kwa mara ya kwanza.

Simba SC wataanza kuitumia VAR katika mchezo Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini utakaopigwa Jumapili (Aprili 17) mwaka huu.

Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu amesema ni furaha kwao kwenda kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza kutumia VAR kwenye uwanja huo ambao umekua ukitumika kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa upande wa Vilabu na timu za Taifa.

“Simba tunakwenda kuwa timu ya kwanza kutumia mfumo wa msaada wa VAR kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa hapa jijini Dar es Salaam.”

“Ni jambo la kheri sana kuwepo kwa VAR uwanjani, nadhani mashabiki wa Simba SC wasubiri kupata burudani siku hiyo ya mchezo.”

“Tayari ‘CAF’ wameshatoa taarifa kuhusiana na uwepo wa matumizi ya VAR kwenye mchezo wetu wa kwanza wa Robo Fainali kwenye uwanja huo,” amesema Mangungu.

Kwenye mchezo huu mwamuzi wa kati atakuwa ni Haythem Guirat kutoka Tunisia, akisaidiwa na mwamuziki msaidizi namba moja, Khalil Hassani (Tunisia), mwamuzi namba mbili Samuel Pwadutakam (Nigeria) na mwamuzi wa akiba ni Sadok Selmi (Tunisia).

Mwamuzi wa teknolojia ya usaidizi kwa njia ya video (VAR) atakuwa ni Ahmed Alghandour (Misri) na msaidizi wake ni Youssef Elbosaty (Misri) na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuitumia.

Polisi Tanzania yaibana Simba SC Ushirika-Moshi
Kocha Orlando Pirates aihofia Simba SC Kwa Mkapa