Wakati Simba SC ikiwa kwenye mchakato wa kumtangaza kocha wao mpya mara baada ya kuachana na Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, uongozi wa klabu hiyo umewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa timu hiyo kwa kuweka wazi kuwa kikosi chao kiko kwenye mikono salama.
Simba SC juzi Jumanne (Novemba 07) ilitangaza kufikia makubaliano ya pande mbili ya kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu Robertinho kwa kile kilichoelezwa kiwango kibovu cha timu hiyo hususani kipigo cha mabao 5-1 walichokipata kutoka kwa watani zao wa jadi, Young Africans.
Pamoja na taarifa hiyo, Simba SC pia walitangaza kikosi hicho kwa sasa kitakuwa chini ya kocha wao wa makipa, Daniel Cadena na kusaidiwa na Selemani Matola.
Makocha hao wanatarajiwa kuiongoza Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa baadae leo Alhamisi (Novemba 09) dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema: “Tunaelekea katika mchezo mgumu dhidi ya Namungo ambapo kikosi kipo chini ya kocha Daniel Cadena ambaye amekabidhiwa jukumu la kuiongoza timu yetu kwa kipindi hiki.
“Niwatoe hofu Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuwa, huyu ni kocha mwenye wasifu na uwezo mkubwa, hivyo wakati huu tukitafuta kocha wa kudumu tuwe na imani kuwa Simba yetu ipo katika mikono salama.”