Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, umeweka wazi mipango na matarajio yao kwa msimu wa 2021/22 ambao unaanza rasmi leo Jumatatu (Septemba 27) katika viwanja vitatu tofauti.
Simba SC itashuka dimbani kesho Jumanne (Septemba 28) kwa kucheza dhidi ya Biashara United Mara mjini Musoma mkoani Mara kwenye uwanja wa Karume.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC Barbara Gonzalez, amesema wanakwenda kuanza msimu mpya wa 2021/22 kwa mambo mapya jambo ambalo litakuwa ni rekodi kwa timu yao.
Barbara amesema kuwa wanatambua juu ya umuhimu wa michezo yao ya Ligi Kuu pamoja na mipango iliyopo, hivyo watakuwa tofauti katika kila jambo.
“Nadhani ni msimu mpya, hapo sisi tunapaswa kuwa na mambo mapya, kwetu kila kitu ni kipya, kuanzia mbinu, wachezaji wetu nao wana mipango mipya.”
“Jambo la msingi kwa sasa ni mashabiki kuendelea kuwa nasi bega kwa bega kwani Simba ni timu kubwa, hivyo inahitaji kuwa na matokeo makubwa pia katika yale ambayo yanafanyika,” amesema Barbara.
Simba SC ilipoiteza mchezo wa Ngao ya Jamii kwa kufungwa na Young Africans bao 1-0 Jumamosi (Septemba 25), halia mbayo imechukuliwa kama fundisho la kupambana kuelekea michezo ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22.
Michezo ya ufunguzi wa Ligi Kuu 2021/22 inayopigwa leo Jumatatu (Septemba 27), Mtibwa Sugar watapambana na Mbeya Kwanza FC, Namungo FC dhidi ya Geita Gold na Coastal Union dhidi ya Azam FC.
Kesho Jumanne (Septemba 28) Dodoma Jiji FC dhidi ya Ruvu Shooting, Mbeya City dhidi ya Tanzania Prisons na Biashara United Mara dhidi ya Simba SC.
Keshokutwa Jumatano (Septamba 29) Polisi Tanzania dhidi ya KMC FC na Kagera Sugar dhidi ya Young Africans.