Uongozi wa Klabu ya Simba SC umethibitisha kuachana na Kocha wa Magoli Kipa Tyron Damons, ambaye alijiunga na klabu hiyo mwishoni mwa mwaka 2021.
Damons aliajiriwa Simba SC, akichukua nafasi ya Kocha Adel Zrane, ambaye alisitishiwa mkataba wake, baada ya klabu hiyo kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2021/22, kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy jijini Dar es salaam.
Simba SC imeto ataarifa za kuagana na Kocha huyo kutoka Afrika Kusini, huku ikithibitisha kuwa, amepata kazi kwenye klabu ya Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka nchini humo ‘PSL’.
“Klabu ya Simba inamtakia kila la heri Kocha wa magoli kipa ambaye anataraji kuondoka klabuni kwetu mwishoni mwa msimu huu.”
“Tyron amepata kazi kunako klabu ya Orlando Pirates ya nchini kwao Afrika Kusini na tayari amewasilisha ombi la kutaka kuondoka klabuni kwetu na kujiunga na miamba hiyo ya Afrika Kusini.”
“Tayari mchakato wa kutafuta mrithi wa Tyron umeanza na dhamira na kumpata kocha mpya wa magoli kipa kabla ya kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya wa mashindano. #NguvuMoja” imeeleza taarifa ya Simba SC