Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umetoa onyo kali kwa wanaojihusisha na uuzaji au usambazaji wa jezi zenye nembo ya klabu hiyo tofauti na Mzabuni Kampuni ya Vunja Bei.
Kampuni ya Vunja Bei iliingia mkataba wa miaka miwili na Simba SC wenye thamani ya shilingi Bilioni 2 ya kutengeneza na kuuza jezi kwa kipindi cha miaka miwili.
Leo mchana Simba SC imetoa taarifa ya onyo kwa wanaoendelea kuuza na kusambaza vifaa vya michezo vya klabu hiyo tofauti na Mzabuni Kampuni ya Vunja Bei.
Kama itakumbukwa vyema Aprili 20, 2021 akitangaza rasmi mkataba huo Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez alisema ni mkataba wa kihistoria kwa Tanzania, kwani haijawai kutokea kuingiwa kwa mkataba wenye thamani kubwa kama hiyo Afrika Mashariki na Kati.
Gonzalez alisema kuwa, mkataba huo utakuwa umempa nafasi ya kuuza bidhaa zote zinazohusiana na Simba kama jezi, kofia, soksi na vifaa vingine vya klabu hiyo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Vunjabei Group Limited, Fred Fabian Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei aliishukuru klabu ya Simba kwa kuichagua kampuni hiyo kwa sababu kulikuwa na makampuni mengi, lakini waliamua kuipa nafasi kampuni yao kwa kuthamini ubora wa kazi zao.
Pia aliwaomba mashabiki wa Simba kuanza utaratibu wa kununua bidhaa rasmi za klabu ili kupata vifaa halisi na vyenye ubora mkubwa.