Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema malengo makuu ya klabu hiyo msimu huu 2022/23, ni kutinga Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kurejesha heshima ya Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.
Simba SC imeshatanguliza mguu mmoja hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kuafuatia kuongoza 3-1 dhidi ya Primeiro De Agosto ya Angola, huku ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 11 sawa na Young Africans iliyozidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.
‘Try Again’ amesema Uongozi wa Simba SC umejipanga kuyasimamia malengo hayo kwa vitendo na hawana sababu ya kukubali kushindwa kurahisi, wakati tayari kikosi chao kimeonesha kila kitu kinawezekana.
Amesema msimu uliopita mambo mengi yalisababisha mambo kuwaendea kombo ikiwa pamoja na kukabiliwa na wachezaji kadhaa majeruhi, lakini msimu huu mambo yameanza kuonekana kuwa mazuri na wana uhakika wa kikosi chao kitafikia malengo.
“Sio kuingia tu Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika lengo letu ni nusu fainali na kuchukua makombe yote ya hapa nyumbani, Yanga walitufunga msimu uliopita sababu tulikuwa na majeruhi wengi msimu huu wasahau hilo”
“Uongozi unafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tunayasimamia malengo yetu kwa vitendo, tunaamini inawezekana kwa sababu dalili njema huonekana asubuhi,”
“Tunachosisitiza kwa Mashabiki na Wanachama wetu ni kuendelea kuwa na imani na Uongozi sambamba na Kikosi chao kila kinapokuwa na mtihani wa kusaka ushindi kwenye michezo ya Nyumbani na Kimataifa.” Salim Try Again
Simba SC ipo kwenye maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Primeiro De Agosto ya Angola, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Oktoba 16) saa kumi jioni, huku ikitarajia kukutana na Young Africans Oktoba 23 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.