Uongozi wa klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC, umetoa ufafanuzi wa kuajiriwa kwa Kocha Hitimana Thiery na kuongezwa kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo ambalo linaongozwa na Didier Gomes.
Hitimana Thiery alitambulishwa rasmi jana Ijumaa (Septemba 10) jioni, huku ikidaiwa kuajiriwa kwake klabuni hapo kumetokana na changamoto ya elimu ya kocha Gomes, ambayo haitoshi kukaa kwenye benchi la Simba kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amesema Gomes alipendekeza kuajiriwa kwa msaidizi mwingine katika benchi lake la ufundi, na ombi hilo alilifanya kabla ya kuibuka kwa taarifa za kusitishwa kukaa kwenye benchi la ufundi katika michuano ya kimataifa.
“Ni jambo la kawaida kwa timu kubwa kuwa na makocha wasaidizi zaidi ya mmoja kutokana na mahitaji ya timu hivyo, tumeamua kuongeza nguvu katika timu kwa kuwa na mtu wa aina ya Thierry,” amesema Barbara.
Kwa upande wa Kocha Gomez amesema amefurahishwa na ujio wa Hitimana Thiery, ambaye ni kocha mwenye daraja la juu, huku akiamini atamsaidia kufikia malengo kuelekea msimu wa 2021/22.
“Wakati nikija Afrika kwa mara ya kwanza nilianzia Rwanda na Rayon Sports ndiyo ilikuwa timu ya kwanza, nakumbuka nilikuwa mkali sana enzi zile na Hitimana alikuwa anasaidia kupooza joto kidogo. Ni mtu mzuri, ni kocha wa viwango, amesema.”
Hitimana ni msomi wa Shahada ya Uzamili katika masuala ya fedha aliyopata nchini Ubelgiji na ana leseni ya ukocha daraja A inayotolewa na CAF.