Uongozi wa Klabu Bingwa Tanznaia Bara Simba SC, umewataka Young Africans kuwasilisha ofa ya kuwasajili viungo Claotus Chama kutoka Zambia na Gerson Fraga kutoka Brazil, ili kuwaridhisha mashabiki na wanachama wao katika kipindi hiki cha dirisha la usajili kuelekea msimu wa Ligi Kuu 2020/21.

Simba wametoa wito huo kwa watani zao wa jadi, kufuatia kuibuka kwa sakata la kiungo mshambuliaji Bernard Morrison kutoka nchini Ghana, kutangazwa kutua Msimbazi mwishoni mwa juma lililopita akitokea Young Africans.

Young Africans wenye maskani yao makuu kwenye makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani wamekua wakitajwa kusuka mipango ya kuwasajili viungo wa Simba Chama na Fraga, ili kulipa kisasi.

Taarifa hizo zilikolezwa zaidi juzi baada ya Young Africans kufanikiwa kuipata huduma ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mbatha Mazingiza, zikidai kituo kinachofuata kwa Chama ni Jangwani kuungana na bosi huyo kutoka Afrika Kusini.

Mshauri wa Mwekezaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohammed “Mo” Dewji, Crescentius Magori ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, amesema watani zao wanaweza kuwasajili wachezaji hao kwa sasa kama tu watakubaliana dau wanalolitaka.

Magori amesema kuwa wachezaji hao bado wana mikataba na Simba na kwamba Chama ambaye amekuwa akihusishwa zaidi na Young Africans, ana uhakika huo kwa kuwa mchezaji huyo alitia saini mkataba wake mbele yake kipindi yeye akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo (CEO).

“Kama wanamtaka waje mezani, hatukatai kumuuza, endapo wana Dola 800,000 walete tutawauzia, kwani bado tuna mkataba wa mwaka mmoja naye,” Magori alisema.

Nakuongeza kuwa wakati huu Chama akiwa kwao Zambia kwa mapumziko mafupi, amemueleza kuna watu wamekuwa wakimfuata wakala wake kutaka huduma yake.

Kwa upande wa Fraga, ambaye kwa sasa yupo kwao Brazil kwa mapumziko mafupi, amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa ameuandikia barua uongozi wa Klabu ya Simba kuomba kuondoa kama ambavyo inadaiwa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Amesema bado yupo Simba na hajamaliza mkataba, na sasa yupo kwao kwa mapumziko mafupi na atarejea mapema kabla ya muda wa kuingia kambini.

“Hizo taarifa za kuandika barua si kweli, mimi ni mchezaji halali wa Simba, mkataba wangu umebaki miezi sita, nitarudi kuitumikia timu yangu kwa msimu ujao,” alisema kiungo huyo.

Amchinja mtoto, kisa wivu wa mapenzi
Maandamano yamng'oa Waziri Mkuu Lebanon