Uongozi wa klabu bingwa Tanzania bara wekundu wa Msimbazi ‘Simba SC’, umewashukuru na kuwapongeza mashabiki walijitokeza uwanja wa taifa Dar es salaam, kushuhudia mpambano dhidi ya Young Africans, Septemba 30.

Shukrani na pongezi kwa mashabiki wa klabu hiyo, zimetolewa na kaimu rais wa mabingwa hao Salim Abdallah (Try Again), ambapo amesema ni jambo jema kuona mashabiki wa Simba wanazidi kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuendelea kuipa hamasa timu yao.

“Ni jambo na faraja kuona mashabiki wakiendelea kuipa hamasa timu, wachezaji wamefarijika na walihitaji kurejesha fadhila kwa kupata ushindi, lakini haikuwa hivyo,”

“Ninaendelea kuwataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa pamoja na kuiamini timu yao, ambayo ina jukumu zito la kutetea ubingwa wa Tanzania bara msimu huu,” alisema Try Again.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo, amesema anaamini timu ya Simba itafanikisha lengo la kupambana na kurejea kileleni mwa msimamo mwa ligi kuu, kutokana na kuwa na kikosi, ambacho kina kila sababu ya kufanya hivyo.

Related imageSalim Abdallah (Try Again)

“Simba ina kikosi kipana ambacho kina uwezo wa kucheza na yoyote ndani na nje ya nchi, suala la timu nyingine kuongoza msimamo wa ligi kuu kwa sasa halitupi shida, tunaamini wakati utafika tutarejea kileleni ili kuonyesha hadhi na ubora wa kikosi chetu,”aliongeza.

Kwa sasa Mtibwa Sugar wanaongoza msimamo wa ligi kuu ya soka Tanzania bara wakiwa na alama 16, wakifuatiwa na Mbao FC wenye alama 14, Young Africans inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 13, sawa na JKT Tanzania, Singida Utd na Coastal Union.

Azam FC ipo kwenye nafasi ya saba ikiwa na alama 12 huku mabingwa watetezi Simba SC wanashika nafasi ya nane kwa kuwa na alama 11.

Matokeo ya darasa la saba yafutwa
Maafa ya Tetemeko Indonesia yafikia watu 1,200