Hatimaye Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morisson amejiunga na wachezjai wenzake wa Simba SC, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC.
Morisson alipatwa na kadhia saa chache baada ya mchezo wa Simba SC dhidi ya Young Africans Jumamosi (April 30), huku akidaiwa kukwaruzana na baadhi ya Mashabiki maeneo ya Chang’ombe jijini Dar es salaam.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, amethibitisha taarifa za Morisson kujiunga na wachezaji wenzake kambini, tayari kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Namungo FC utakaopigwa mjini Lindi kesho Jumanne (Mei 03).
Ahmed amesema Kiungo huyo alikua sehemu ya mazoezi ya kikosi cha Simba SC jana Jumapili (Mei Mosi) majira jioni baada ya kuachiwa na Polisi.
Wakati huo huo Kikosi cha Simba SC kimewasili mkoani Mtwara leo Jumatatu (Mei 02) asubuhi, na kisha kuelekea mkoani Lindi, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 22 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC kesho Jumanne (Mei 03).
Simba SC imethibitisha taarifa za kuwasili kwa kikosi chao mkoani Mtwara na kisha kuanza safari ya kuelekea Lindi, kupitia kurasa zake za mitandao ya Kijamii.
Taarifa ya Simba SC imeeleza: “Kikosi kimefika mkoani Mtwara. Kesho kitacheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC kwenye uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi. #NguvuMoja”
Simba SC ipo nafasi ya pili katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42, huku ikiachwa kwa tofauti ya alama 13 dhidi ya vinara Young Africans yenye alama 55.