Klabu ya Simba  imewasilisha barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka Yanga iwalipe dola za Marekani 60,000 (sawa na Sh milioni 130) kwa madai ya kumsajili mchezaji Hassan Kessy kinyume na taratibu.

Kesi ya madai ya Simba dhidi ya Yanga inatarajiwa kunguruma Jumamosi ya wiki hii pale Kamati ya Sheria na Hadhi kwa wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Richard Sinamtwa itakapokutana.

Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa Sheria na uanachama wa TFF, Eliud Mvela alisema jana kuwa Simba imewasilisha barua ya madai kwa Shirikisho hilo juzi na hivyo Jumamosi kesi hiyo itatolewa ufumbuzi.

Kessy, hivi karibuni alishindwa kuitumikia Yanga katika mashindano ya kimataifa kutokana na Simba kugoma kutoa barua ya kuthibitisha kumalizana na beki huyo kwa madai kuwa alikiuka makubaliano kwa kusaini mkataba mwingine kabla ya aliokuwa nao kumalizika.

Hata hivyo wiki iliyopita Kamati ya Sheria na hadhi ya wachezaji ilimuidhinisha Kessy kuichezea Yanga kwa madai ya kulinda kipaji chake na kwamba kwa vile ni madai ni lazima Kessy acheze ili apate fedha ya kuilipa Simba ambayo tayari imefungua kesi ya madai ikitaka kulipwa fedha hizo kama fidia.

Simba inadai kuwa katika mkataba huo yalikuwepo makubaliano ya mmojawapo kati ya klabu au mchezaji akivunja mkataba, basi aliyevunja mkataba ni lazima amlipe mwenzake dola 60,000 ambazo Kessy anatakiwa kuzilipa.

“Suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Yanga kabla ya kumaliza mkataba wake. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016,” alisema Mvela.

Mbali na kesi hiyo, Mvela alisema kuwa kamati hiyo pia itapitia madai ya kocha wa zamani wa Simba Richard Amatre aliyewasilisha kuitaka Simba imlipe Sh milioni 17.2 ikiwa ni sehemu ya mshahara wake la sivyo anatinga FIFA ili imsaidie kupata haki zake kwa Wekundu hao wa Msimbazi.

Mvela alisema kuwa Simba imekuwa ikimzungusha Amatre tangu mwaka 2014 ilipomvunjia mkataba wake.

Kwa nyakati tofauti, Amatre aliwahi kufanya kazi katika Klabu ya Simba akiwa kocha msaidizi wa waliowahi kuwa makocha wakuu wa klabu hiyo Mganda Moses Basena na Mserbia Milovan Cirkovic.

Amatre alisema kiasi hicho cha fedha anachoidai Simba ni fidia inayotokana na hatua ya klabu hiyo kuvunja mkataba wake sambamba na aliyekuwa bosi wake, Milovan.

Coastal Union Kuzibana Simba, Yanga, Kagera Sugar Na Mbeya City
Video: Wapenzi wa jinsia moja 'wazaa' mapacha watatu