Kiungo Mshambuliaji wa Coastal Union, Ahmed Simba amesema ametazama za mchezo karibuni za wapinzani wa Young Africans, USM Alger na kugundua ni timu inayofungika kirahisi hivyo Wananchi wakikomaa wanawafunga vizuri tu kwenye michezo miwili watakayocheza ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans itawakaribisha USM Alger keshokutwa Jumapili (Mei 28) katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Fainali utakaopigwa kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam na kurudiana Juni 3 nchini Algeria.
Simba amesema sliangalia mechi mbili za Nusu Fainali dhidi ya Asec Mimosas na kugundua timu hiyo inafanya makosa mengi kwenye safu yake ya ulinzi hivyo kama washambuliaji wa Young Africans wakiwashambulia kwa nguvu basi watafunga mabao mengi.
“Sema ni wajanja sana wanapocheza mechi za ugenini wanakuja na mbinu zao niliona jinsi walivyokuwa wakipoteza muda lakini ni timu ambayo ina makosa mengi sana haswa kwa mabeki wake wakikutana na washambuliaji wazuri wanawafunga vizuri sana.”
“Wakienda kule kwao kuwafunga wakiwatangulia basi unakuwa umemaliza mechi,” amesema Simba ambaye kwa sasa ni kocha wa Copco FC inayoshiriki Championship.
Ámesema safu ya ushambuliaji ya Young Africans inahitaji kuongeza umakini ili wakipata nafasi za kufunga waweze kuzitumia kwani wanahitaji sana mabao.