Hatimaye mtanange wa kwanza wa mwaka 2020 uliowakutanisha watani wa Jadi, Simba na Yanga umemalizika jijini Dar es Salaam kwa sare ya 2-2.
Simba walianza kuwapa raha mashabiki wao kupitia mkwaju wa penati ulitundikwa kimyani na Medie Kagere katika dakika ya 42. Ni yuleyule aliyewahi kuiliza Yanga Februari 16, 2019 ambapo goli lake lilikuwa msumari uliwashinda Yanga kuuchomoa hadi mwisho wa mchezo mwaka huo.
Lakini leo, kabla machungu hayajapoa, mchezaji kutoka Congo DRC Deo Kanda aliwachoma msumari mwingine Yanga akipachika goli katika dakika ya 47.
Hata hivyo, Yanga walivuta pumzi wakilipania goli la simba ili wayashushe machungu ya mashabiki wao. Katika dakika ya 50, Mapinduzi Balama alifanikiwa kupachika goli la kwanza na kuufanya mchezo kuwa 2-1. Kama ilivyokuwa kwa Simba, dakika nne baadaye Yanga walijipatia tena goli la kusawazisha kupitia kwa mchezaji wake Mohammed Issa Banka.
Hadi kipyema cha mwisho kinapulizwa, Yanga 2-2 Simba.
Katika mchezo huo, Simba SC walipata kona nane, Yanga SC walipata kona tatu. Lakini Simba walionekana kumiliki mpira kwa 53% dhidi ya 47% za Yanga.
Je, nani anapaswa kupongezwa na nani alaumiwe? Wachezaji lao uwanjani, mashabiki mchezo wao ni endelevu hadi nje ya uwanja. Usikose kuangalia mahojiano na vitimbwi kwenye derby hii ya Dar es Salaam kupitia YouTube Channel ya Dar24 Media.