Katika kile kinachoonekana kuwa mabadiliko katika benchi la ufundi yameanza kuzaa matunda, Simba leo imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 2-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom iliyopigwa kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kipindi cha kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku zikicheza mpira wa kusomana. Licha ya kosa kosa za hapa na pale, timu hizo zilienda mapumziko bila bao lolote.

Mohamed Hussein Tshabalala alitolewa nje ya uwanja kwa machela nafasi yake ikichukuliwa na Abdi Banda, baada kuonekana kuwa amepata maumivu makali kufuatia rafu aliyochezewa na Samwel Kamuntu ambaye alizawadiwa kadi ya njano.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko ya kumuingiza Hassan Kessy badala ya Peter Mwalyanzi, mabadiliko ambayo yalizaa matunda kwani kasi yao iliongezeka na kufanya mashambulizi mengi zaidi yaliyopelekea kupata penati katika dakika 52 baada ya Danny Lyanga kuangushwa kwenye eneo la hatari. Penati hiyo iliwekwa wavuni na Hamis Kiiza katika dakika 54.

Simba iliendelea kulishambulia lango la JKT Ruvu na kufanikiwa kupata bao katika dakika 62 mfungaji akiwa ni Lyanga aliyeunasa mpira na kumpiga chenga kipa baada ya walinzi wa Ruvu kugongana wenyewe.

Kocha wa Simba alimpumzisha pia Lyanga na kumuingiza Paul Kiongera huku JKT Ruvu ikiwapumzisha Kamuntu na Issa Ngao na nafasi zao zikichukuliwa na Saad Kipanga na Amos Edward.

Kwa ushindi huo Simba imeendelea kubaki katika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 33 nyuma ya Yanga yenye 36 na Azam yenye 39

Jukwaa la Wahariri Lamkosoa Nape, mawio lapata mtetezi
Serikali yakanusha uzushi uliosambaa kuhusu Rais Magufuli