Klabu ya Simba wamemsimamisha kiungo wao, Jonas Mkude ambaye hayupo kambini tangu kikosi hicho kilivyo rejea nchini kutoka Afrika Kusini kucheza mechi ya mzunguko wa kwanza dhidi ya Kaizer Chiefs.
Taarifa kutoka Simba zinaeleza siku ya pili baada ya kurejea kutoka kwa Madiba ambayo ilikuwa Jumanne Mei 18, wachezaji wote wa kikosi hicho walirejea kambini ila Mkude hakuwepo tena bila ya sababu maalumu.
Siku aliyokwenda kambini Mkude alitoa sababu ambayo ilimfanya kushindwa kwenda kambini kwa wakati jambo ambalo si kocha, Didier Gomes wala Meneja, Patrick Rwetemamu aliyeikubali. Baada ya Mkude sababu yake kushindwa kukubalika alisimaishwa na kutakiwa kuwa nje ya timu mpaka mchezo wa marudiano na Kaizer utakapopita.
Taarifa zilieleza zaidi kuwa hata mara baada ya mechi na Kaizer kumalizika kiungo huyo amekatiliwa kurudi kambini ili kujiunga na wenzake kuendelea na majukumu yake ya kila siku kama ilivyokuwa hapo awali.
Suala hilo la kinidhamu ambalo bado hawajaliweka wazi Simba kuwa Mkude amefanya nini tayari limepelekwa hadi kamati ya nidhamu ambayo itatoa adhabu yake baada ya kumsikiliza kiungo huyo.