Mabingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ Simba SC wamejizatiti kutetea taji la michuano hiyo, baada ya kutinga kwenye mzunguuko wa nne kwa kuifunga JKT Tanzania.

Kikosi cha Simba SC kilicheza dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania juzi Jumanne (Desemba 14), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Mshambuliaji Kibu Denis.

Katika kuhakikisha wachezaji wanapambana na kuendelea kulishikilia taji la michuano hiyo inayochezwa kwa mfumo wa mtoano, Uongozi wa Simba SC umetenga kiasi cha Shilingi milioni 70 kama Bonasi.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zinaeleza kuwa, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, wameongeza Bonasi katika michuano hiyo kutoka Shilingi Milioni 50 na kufikia Milioni 70 kwa kila mchezo.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, lengo la kuongeza Bonasi hiyo ni kuwaongezea Morali na hali ya kupambana wachezaji ili kuweza kutetea ubingwa wa michuano hiyo.

“Wachezaji wa Simba waliocheza na wale waliokaa Benchi kila mmoja ana uhakika wa kupata bonasi nzuri ya mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho dhidi ya JKT Tanzania ambao tulishinda bao 1-0.”

“Bonasi hiyo ya Sh 70Mil ambayo watapatiwa wachezaji imeongezeka msimu huu, kumbuka msimu uliopita walikuwa wakipata Sh 50Mil.”

“Hiyo itawapa hali ya kujituma na kupambana ili tutetee kombe letu, hiyo bonasi inajitegemea tofauti kabisa na ligi na michuano ya kimataifa.” Imeeleza taarifa hiyo.

Simba SC inashikilia taji la ASFC kwa msimu miwili mfululizo, Msimu wa 2019/20 ilitwaa ubingwa huo kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-1 na msimu wa 2020/21 ilifanya hivyo kwa kuibanjua Young Africans bao 1-0.

Klopp: Sitasajili Januari 2022
Paul Pogba akataliwa FC Barcelona