Mara baada ya Simba kufanikiwa kufuzu kucheza Raundi ya Kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika, baadhi ya Wabongo wakawa wanamtaja mshambuliaji Aristide Bancé wa Al-Masry kuwa ndiye hatari kwa Simba.
Pamoja na sifa hizo za Bance lakini ukweli ni kuwa umri unaonekana kuanza kumtupa mkono staa huyo wa timu hiyo ambayo itacheza na Simba katika hatua inayofuata lakini kuna wachezaji wengine ambao ndiyo wanaotajwa kuwa hatari zaidi.
Wachezaji hao ni Mostafa Mohamed, Ahmed Shoukry na hatari zaidi ni Ahmed Gomaa ambaye amekuwa hatari kwenye kufunga.
Licha ya kuwa wote, Bance na Gomaa wana bao moja kila mmoja katika michuano hiyo lakini ndani ya Misri Gomaa amekuwa na makali zaidi.
SIMBA WAPEWA SIRI
Wakati Simba ikirejea nchini usiku wa kuamkia jana kutoka Djibouti ilipocheza dhidi ya Gendarmerie Nationale, mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amewapa mbinu viongozi wa Simba ambazo wanaweza kuzitumia kuwatoa ‘nishai’ Waarabu hao.
Rage ameliambia gazeti hili kuwa amefurahishwa na matokeo ya Simba kutinga hatua inayofuata ambapo ameshauri kwanza kuwachezesha Waarabu wakati wa jua kali kwa kuwa hawajazoea.
“Kama wanaweza wawachezeshe Waarabu wakati wa jua la saa tisa alasiri, hapa kwetu kuna hali ya joto, itawasumbua.
“Wanaweza kuzungumza na kocha mapema ili kuwafanyisha wachezaji mazoezi ya muda huo, na sheria za Fifa zinaruhusu mechi kuchezwa saa tisa.
“Ukienda kule wenzetu wana fitna sana kwao, lazima mechi ya marudiano itakuwa saa moja usiku kwa kuwa kuna baridi muda huo, hivyo itawapa shida wachezaji wetu, hivyo ni vyema tukawawahi itasaidia sana,” alisema Rage.
INAFUNDISHWA NA NGULI WA ZAMALEK
Straika wa zamani wa Al-Ahly na Zamalek, Hossam Hassan ndiye kocha wa timu hiyo ambaye enzi zake alikuwa maarufu na alikuwa na uwezo mkubwa, alikuwa staa wa timu ya taifa ya Misri pia.
UONGOZI WA SIMBA WAJINADI
Uongozi wa Simba umefunguka kuwa watafanya maandalizi makali kabla ya kukutana na wapinzani hao.
Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Simba, Haji Manara ameliambia Championi Ijumaa kuwa wanawaheshimu Al Masry lakini mikakati yao ni mikubwa.
“Al Masry ni klabu nzuri lakini kamwe huwezi kuwa mkubwa na kufanya vyema katika michuano hii kama utashindwa kuwatoa wakubwa kama hawa, kabla ya mchezo huo tutajipanga kwelikweli kuhakikisha kwamba tunafanya vyema mbele yao.
“Tunawaheshimu kiukweli kwa sababu wanafanya vizuri katika ligi ya kwao Misri lakini nikwambie mwaka huu tumedhamiria kufanya vyema kwenye mashindano yoyote yale, kila mmoja anajua umuhimu wa mchezo huo na naamini tutafanya vizuri,” alisema Manara.