Saa chache kabla ya kushuka dimbani, Simba SC imesema leo Ijumaa (Oktoba 20) itadhihirisha ukubwa wake kwa mashabiki wa soka Duniani kwa kuifunga Al Ahly ya Misri katika hatua ya Robo Fainali ya michuano ya African Football League (AFL).
Wekundu hao wa Msimbazi watachuana na Al Ahly saa 12:00 jioni katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya michuano hiyo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Michuano hiyo itakayozinduliwa leo Ijumaa (Oktoba 20), inashirikisha klabu nane za soka barani Afrika, ambazo ni Simba SC, Al Ahly, TP Mazembe (DRC), Petro de Luanda (Angola), Esperance ya Tunisia.
Timu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo ni Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Wydad AC (Morocco) na Enyimba ya Nigeria.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’, amesema hana Presha yoyote kuelekea mchezo huo licha ya kukiri itakuwa mechi ngumu.
Robertinho amesema wanaiheshimu Al Ahly kwa kuwa ni timu kubwa na ina uzoefu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
“Ninatambua kuwa Al Ahly ni timu bora na ina uzoefu katika michuano mbalimbali barani Afrika, lakini mpira ni dakika 90 za uwanjani tutahakikisha tunapata matokeo chanya.
“Sina Presha na mchezo wa leo licha ya kuwa ni mkubwa, hata mimi nikiwa mchezaji kule Brazil nimewahi kukutana na mechi kama hizi kwa hiyo naifurahla na sina presha,”amesema
Amefafanua kuwa Simba SC inacheza mechi kubwa na Al Ahly, lakini wapo tayari kwa dakika 90 za kushinda mechi hiyo.
Akizungumzia kuhusu kurejea kwa mlinzi Na kati, Henock Inonga ambaye alikuwa majeruhi, Robertinho amesema ni mchezaji bora barani Afrika na kusisitiza kuwa kurejea kwake kutawaongezea nguvu na anategemea kumtumia katika mchezo huo.
Naye Nahodha wa Simba SC, John Bocco, amesema licha ya ugumu watakaoupata katika mchezo huo, lakini uwepo wa mashabiki wengi uwanjani utawaongezea nguvu.
Bocco amesema mashabiki wana mchango mkubwa kuisaidia timu kupata ushindi nao watatumia nafasi hiyo kuhakikisha wanashinda kujivweka katika mazingira mazuri.
“Haitakuwa mechi rahisi, Al Ahly ni timu bora lakini tuna faida ya kucheza nyumbani, kila mchezaji anafahamu umuhimu wa mchezo na tumejipanga kushinda mechi hiyo,” amesema Bocco