Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeeleza kuwa haijatoa tuzo ya mchezaji bora wa mwezi msimu huu mpaka sasa kutokana na kukosekana kwa mdhamini wa tuzo hiyo.
Kwa miaka miwili iliyopita, Simba SC kila mwezi katika miezi inayochezwa ligi imekuwa ikitoa tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki wa timu hiyo iliyokuwa ikidhaminiwa na Kampuni ya Emirate Aluminium ACP.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kampuni hiyo imemaliza mkataba wake msimu uliopita ndio maana kwa sasa hazisikiki tena tuzo hizo zilizokuwa zikipigiwa kura na mashabiki wa Wekundu hao.
“Mkataba wetu na kampuni iliyokuwa ikidhamini tuzo hizo umemalizika tangu mwishoni mwa msimu uliopita ndio maana hazionekani kwa sasa, maana ile tuzo huwa ni zawadi ya mdhamini kwa mchezaji aliyefanya vizuri ndani ya mwezi,” amesema Ally.
Aidha, Ally amebainisha kuwa milango iko wazi kwa kampuni inayotaka kufanya hivyo kama ilivyofanya Emirate Aluminium Septemba 21, mwaka juzi kwa kusaini mkataba wa Sh milioni 300 kwa ajili ya dili hilo.