Ligi kuu ya soka Tanzania bara imeendelea tena hii leo kwa mchezo mmoja wa mzunguuko wa 22, ambao umechezwa kwenye uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro kati ya wenyeji Mtibwa Sugar dhidi ya Wekundu Wa Msimbazi Simba.
Mchezo huo uliokua unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka karibu kona zote za nchi, uliambatana na mvua iliyokua ikinyesha jambo ambalo liliufanya kukosa ladha kutokana na mazingira ya sehemu ya kuchezea ya uwanja wa Jamuhiri kutokua imara.
Hata hivyo dakika 90 zimekamilika kwa kushuhudia wenyeji Mtibwa Sugar ambao maskani yao makuu ni Manungu, Turiani wilaya ya Mvomero wakivurumishiwa kisago cha kufungwa bao moja kwa sifuri, lililofungwa na mshambuliaji kutoka nchini Uganda Emmnuel Okwi dakika ya 23.
Okwi alifunga bao hilo kufuatia mpira wa krosi uliopigwa na Shizya Kichuya na kisha kumfikia John Bocco aliyepiga kichwa na baadae mshambuliaji huyo hatari kumalizia kiulaini.
Kwa matokeo hayo yanaifanya Simba kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha alama 52 na kuendelea kuwaacha wapinzani wao katika soka la Bongo Young Africans wenye alama 46 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.