Hatimaye Klabu ya Simba imeandika tena historia kwa kuingia katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Mabingwa barani Afrika, baada ya kufanikiwa kuizamisha rasmi klabu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika mchezo uliomalizika muda mfupi uliopita jijini Dar es Salaam.
Hii inakuwa mara ya pili kwa klabu hiyo ya Msimbazi kutinga katika hatua hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Mshambuliaji Clatous Chama ndiye aliyefanikisha tena kupachika goli la pili katika dakika ya 90 ya mchezo, goli lililoipa uhakika Simba kutinga katika hatua ya pili, akiongeza idadi ya magoli baada ya goli la kwanza na la kusawazisha lililofungwa na Muhammed Hussein katika dakika ya 35.
Awali, AS Vita walikuwa wa kwanza kupata goli lao la pekee katika dakika ya 12, hali iliyowapa nguvu ya kuendelea kushambulia, kabla ya kutulizwa na goli la M. Hussein katika dakika ya 35
Ni chama huyuhuyu ambaye alipachika goli la tatu dhidi ya Nkana, goli ambalo liliwavusha wekundu wa Msimbazi na kuingia katika hatua ya mzunguko wa 16, ikiwa katika kundi D.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ushindi huo, kocha wa Simba, Patrick Aussems aliwapongeza wachezaji wake na kuelezea furaha yake kwa jinsi ambavyo wamefanikiwa kufikia lengo ambalo ni kuingia katika hatua ya robo fainali.
“Leo ilikuwa mechi ngumu na kulikuwa na nafasi nyingi za kushinda kwani ilikuwa ni mechi ya wazi, lakini ushindi ulianza na Al Ahly,” alisema Kocha Patrick Aussems.
“Kwa Simba na kwa Tanzania ni kitu kizuri, lengo lilikuwa kufika katika hatua ya robo fainali. Unaweza kushangaa, sisi tulikuwa timu ambayo ilifungwa 5-0 mara mbili, lakini tumefanikiwa kuvuka. Hii inapaswa kuwa furaha kwa soka la Afrika Mashariki,” alisema Aussems.
Kocha huyo ameeleza kuwa kazi ya Haruna Niyonzima ilikuwa ya kutukuka na ametoa mchango mkubwa katika kufanikisha ushindi wa leo.
Kwa upande wa Kocha wa AS Vita, aliwapongeza Simba kwa ushindi akiielezea kuwa ni timu nzuri iliyofanikisha lengo na kwamba wao walishindwa kutumia vizuri nafasi nyingi walizozipata.
“Tulikuja hapa kushinda, lakini tumeshindwa, tunaipongeza Simba,” amesema kocha wa AS Vita.
Kwa matokeo hayo, Simba wameingia robo fainali ikiwa na alama 9, ikiwa nafasi ya pili baada ya Al Ahly yenye alama 10.