Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Wekundu Wa Msimbazi Simba, wameshindwa kuwa timu ya kwanza kuvunja mwiko kwa kuwabanjua maafande wa jeshi la Magereza Tanzania Prisons, ambao wanaendelea kuwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo tangu kuanza kwa msimu huu wa 2019/20.
Simba wameshindwa kutimiza mpango huo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam baada ya kuonyeshwa upinzani mzito na wa kweli dhidi ya maafande hao, ambao maskani yao makuu yapo jijini Mbeya.
Mbali na kupewa nafasi ya kushinda mchezo wa leo, bado Simba walikua na wakati mgumu wa kuzuia mashambulizi ya maafande hao, walionekana kujizatiti vilivyo muda wote na kuonyesha upinzani wa kweli, hadi kumaliza dakika 90 wakiambulia matokeo ya bila kufungana.
Suluhu hiyo imewafanya Simba kugawana alama moja moja na Prisons ambao mpaka sasa hawajapoteza mchezo wowote kwenye ligi.
Alama hiyo moja imewafanya Simba kuendelea kukaa kileleni wakiwa na alama 22 huku wakiwa wamepoteza mchezo mmoja mpaka sasa.
Prisons mpaka sasa imecheza jumla ya mechi 11 na wakienda sare michezo saba huku wakishinda nne na wakiwa na alama 19 kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa ligi.