Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, umelazimika kuwafanyia vipimo vya Covid-19 wachezaji wao wote, ili kuepuka hujuma ambao huenda wakakutana nazo kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.
Simba SC, itaanzia ugenini mjini Gaberone, Botswana Jumapili (Oktoba 17), kisha itarejea nyumbani jijini Dar es salaam kucheza mchezo wa mkondo wa pili, Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 22.
Uongozi wa umechukua tahadhari ya kuwafanyia vipimo vya Covid-19 wachezaji na maafisa wengine watakaokua safarini nchini Botswana, kuepuka majibu feki ya vipimo ambayo yamekua yakiwalenga wachezaji muhimu ili wasicheze.
Meneja wa Simba SC, Patrick Rweyemamu, amesema vipimo hivyo vimefanyika katika Hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es salaam na kila mchezaji amekutwa yupo salama.
“Wachezaji wetu pamoja benchi la ufundi wamepimwa Covid-19 tayari kwa maandalizi ya safari kuelekea Botswana.”
“Kupima Covid-19 kabla ya safari kutoka nchi moja hadi nyingine ni utaratibu uliowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo.
“Kikosi kinaelekea Botswana tayari kwa mchezo wa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galax utakaopigwa Jumapili, Oktoba 17.” amesema Rweyemamu
Mshindi wa Jumla ya mchezo kati ya Simba SC dhidi ya Jwaneng Galaxy, atafuzu kucheza hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na atakayepoteza ataangukia kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho hatua ya mtoano.